‘Ma-Pro’ wambeba Kocha Luc Eymael, Yanga 3-1 Singida United

Hot Michezo

SINGIDA, TANZANIA

KIKOSI cha Yanga chini ya ocha wake mpya Mbelgiji Luc Eymael, leo kimeonja ladha ya ushindi na kuzika jinamizi la vipigo mfululizo, baada ya kuichapa Singida United ya Singida mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Liti (zamani Namfua), mjini Singida.

Kabla ya ushindi huo, Eymael alifungwa mara mbili akiiongoza Yanga kukubali kuchapwa katika mechi mbili, akianza na kipigo cha 3-0 kutoka kwa Kagera Sugar, kisha kulala bao 1-0 dhidi ya Azam FC – mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Yanga katika mechi dhidi ya Singida United


Wakicheza mechi ya tatu tangu Eymael asaini kandarasi ya kuino Yanga kwa miezi 18, Wana Jangwani hao walikuwa moto wa kuotea mbali leo, huku nyota wao mpya Benard Morrison raia wa Ghana, akionesha unyumbulifu wa hali ya juu.

Yanga ilianza kuhesabu mabao yake mapema dakika ya 12, kupitia kwa nyota wa kimataifa wa DRC, David Molinga, aliyewafungia bao la uongozi kunako dakika ya 12, lililodumu hadi filimbi ya mapumziko ya pambano hilo.

Kipindi cha pili, Yanga ikaongeza mabao mawili kupitia nyota wake wapya wawili waliosajiliwa kipindi cha dirisha ndogo, Haruna Niyonzima – nyota wa kimataifa wa Rwanda alifunga bao la pili dakika ya 58, kabla ya mu-Ivory Coast Yikpe Gnamien kufunga la tatu dakika ya 78.

Bao la kufutia machozi la Singida United, inayonolewa na Ramadhani Nswanzurwimo, lilifungwa na Six Mwasekaga dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho.

Kwingineko, Azam FC wakiwa ugenini mjini Shinyanga, wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao Mwadui FC, pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini humo. Bao la Azam FC limefungwa na Shaaban Idd ‘Chilunda.’

BIMA BANNER

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *