MAMA aliyegongwa na gari la JWTZ, amwangukia Waziri Dk. Hussein Mwinyi

Habari Hot

ARUSHA, TANZANIA

MAMA mnyonge, Nailejileji Abel Laizer (40), aliyetelekezewa watoto wawili na mumewe, aliyemkimbia baada ya kugongwa na gari la Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Monduli, akidhaniwa amekufa, amemwangukia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, akimuomba amsaidie.

Nailejileji aliyegongwa na gari hilo Juni, 2010 na kupewa hadhi ya Balozi kutokana na kukaa muda mrefu katika Hospitali ya Selian, mbali ya kutoka akiwa na ulemavu wa kudumu, amedai anamshukuru Msamaria aliyemsaidia baada ya kumkuta analia, kwa kuambiwa atakatwa mguu.

Akizungumza kwa masikitiko hivi karibuni, Nailejileji alisema: “Mwanajeshi yule tangu anigonge na mguu wangu kusagika vibaya nikiwa kwenye bodaboda Monduli, hakuona ubinadamu wala umuhimu wowote wa kuniuguza na kunijulia hali, toka Juni, 2010 hadi leo hii.

Nailejileji Abel Laizer (40), Mama aliyegongwa na gari ya Jeshi (JWTZ), anayemwangukia Waziri Dk. Hussein Mwinyi.

“Msamaria alipoona nalia, kuwa nitakatwa mguu alimwambia ndugu yangu tafuteni Hospitali yoyote inayoweza kumfanya mguu usikatwe na kuahidi atanisaidia, jambo ambalo sitamsahau msamaria yule, ila namshangaa mwanajeshi yule kukosa ubinadamu,” alisema Nailejileji.

Alipoulizwa kwa nini anaamini Waziri Dk. Mwinyi atamsaidia, mwanamke huyo alisema: “Naamini JWTZ ni Jeshi ambalo lipo kwa ajili ya faida ya ulinzi wetu wananchi, hivyo Waziri Dk. Mwinyi ambaye ni Kiongozi wake, hata mimi ni mwananchi wake, isipokuwa Mwanajeshi yule aliyenigonga na kunitelekeza, hana Ulinzi wa Wananchi.

“Pia naamini kwamba, Dk. Mwinyi anaweza kunionea huruma, maana nimekuwa mlemavu sina cha kufanya pamoja na kutelekezwa na watoto wawili, lakini yeye akitaka amfahamu aliyenigonga ni nani, na gari lile aina ya ‘Defender,’ hashindwi atamfahamu mapema,” alisema.

Uchunguzi umebaini, Nailejileji hivi karibuni alifika Kituo cha Polisi Monduli ili kufuatilia PF3 na faili lililofunguliwa kuhusu kugongwa kwake, lakini mmoja wa viongozi wa Usalama Barabarani ambaye hakutaka jina lake litajwe, maana siyo msemaji, alidai kuwa, yeye ni Mgeni, hivyo ampe muda afuatilie atamtaarifu.

Mbali ya kuwasiliana na watu wa Usalama, Nailejileji inadaiwa anawasiliana na Viongozi wa Hospitali ya Selian ili kupata Nyaraka zinazoonesha Mwenendo wa Matibabu yake akiwa hospitalini hapo tangu Juni, 2010, ambapo Kiongozi mmoja na Kaka yake walithibisha hilo.

Nailejileji amedai, anawaamini kwa Kiwango kikubwa viongozi wa usalama, anangoja ahadi hiyo ikishindikana atakwenda kwa Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, IGP Simon Sirro na hatimaye, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, ili kupata haki yake.

BIMA BANNER

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *